Skip to content
Advertisements

Mambo 10 yaliyompa cheo kinara makinikia

ALIYEKUWA mwenyekiti wa kamati teule ya kwanza ya Rais iliyofichua upotevu mkubwa wa mapato katika usafirishaji wa mchanga wa madini (makinikia) kwenda nje ya nchi, Prof. Abdulkarim Mruma, – 

ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kampuni ya Kuhifadhi Mafuta (TIPER) huku wachambuzi wa masuala ya uongozi wakitaja mambo 10 kuwa chanzo cha uteuzi wake. 
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu jana, ilieleza kuwa Rais Magufuli amemteua Mruma kushika wadhifa huo akiwa ndiye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania. 
Wengine walioteuliwa jana ni Prof. Joseph Buchweshaija kuwa Mwenyekiti wa Kampuni ya Puma Energy Tanzania Ltd akitokea kuwa Naibu Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) na Prof. Evaristo Joseph Liwa kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ardhi (Ardhi University) kuchukua nafasi ya Prof. Idrissa Mshoro ambaye amestaafu. 
Taarifa hiyo ya Ikulu ilieleza kuwa uteuzi wa Mruma na wenzake ulianza mara moja Agosti 17, 2017. 
Mruma ameteuliwa kushika cheo hicho ikiwa ni takribani miezi mitatu imepita baada ya ripoti ya kamati yake iliyohusisha wataalamu wanane kufichua namna wasafirishaji wa makinikia walivyokuwa wakiikosesha serikali kiasi kikubwa cha mapato kutokana na utoaji wa taarifa zisizokuwa sahihi juu ya kile kilichomo ndani ya makontena ya mchanga huo. 
Katika ripoti hiyo ambayo Mruma aliikabidhi kwa Rais Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam, Mei 24 mwaka huu, ilibainika kuwa makontena 277 ya makinikia yaliyochunguzwa wakati yakiwa yameshikiliwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam, yalikuwa na kiasi kikubwa cha madini tofauti na ripoti zilizokuwa zikiwasilishwa. 
Ilielezwa kuwa tofauti hiyo iliikosesha nchi mapato makubwa kutokana na kasoro ya kiwango cha madini na aina ya madini yaliyokuwa yakisafirishwa, yakiwamo ya dhahabu, shaba, fedha na yale ya metali mkakati kama lithium. 
Kamati hiyo ilibaini kuwa thamani ya madini yote katika makinikia kwenye makontena 277 yaliyochunguzwa yalikuwa na thamani ya Sh. triloni 1.339, ambazo serikali ilikuwa haipati chochote katika mrabaha. 
Wakizungumza na Nipashe kwa nayakati tofauti jana, baadhi ya wachambuzi walitaja mambo 10 kuwa chanzo cha Mruma kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tipper. 
Aidha, kwa mujibu wa wachambuzi, mambo hayo yaliyombeba Prof. Mruma yalijidhhirisha wazi wakati alipoiongoza kamati iliyochunguza usafirishaji wa makinikia nje ya nchi. 
“Mbali na utaalamu mkubwa alio nao katika masuala ya jiolojia, sababu nyingine iliyomfikisha Mruma alipo sasa ni pamoja na uadilifu aliouonyesha wakati akiiongoza kamati teule ya Rais kuchunguza masuala ya makinikia,” mmoja wa wachambuzi aliiambia Nipashe jana na kuongeza: 
“Kama angeyumba kwa kushawishiwa na yeyote ili yeye na wenzake wapindishe ukweli, ni wazi kwamba uadilifu wake ungetiliwa shaka na leo hii asingekumbukwa na Rais katika uteuzi wa nafasi hiyo ya juu Tipper.” 
Aidha, mambo mengine yaliyotajwa kuwa chanzo cha Mruma kuteuliwa na Rais Magufuli katika wadhifa huo mpya wa sasa ni pamoja na ujasiri; uzalendo kwa taifa; uzoefu; sifa ya uongozi bora; umakini; nidhamu ya kazi; msimamo thabiti; kupenda kufanya kazi kwa moyo mmoja na pia kuwa muumini wa kufanya kazi kama timu pasi na kutanguliza umimi. 
“Mruma ni msomi… na pia ni mchapakazi, asiyeyumbishwa katika kusimamia kile anachoamini kuwa ni sahihi kwa maslahi mapana ya taifa. Sifa zote hizo ndizo Rais huzitaka karibu kwa kila mtu anayemteua ili kufikia malengo ya kuwafikishia maendeleo Watanzania,” alisema mchambuzi mwingine na kuongeza: 
“Kazi kubwa na nzuri aliyoifanya Mruma na wenzake katika kamati ya kuchunguza makinikia imedhihirisha kuwa anafaa. Ndiyo maana Rais amemteua kushika cheo hicho kipya cha kuiongoza Tipper.” 
Wakati akipokea ripoti ya kamati ya Mruma na pia ya kamati ya pili iliyoongozwa na Profesa Nehemia Osoro, Rais Magufuli alieleza namna alivyoridhishwa na utendaji wa wote wawili kwa nyakati tofauti, huku akitaja baadhi ya mambo yaliyotajwa na wachambuzi kuwa chanzo cha kuteuliwa kwa Mruma. 
SIFA ZA MRUMA ALIZOGUSIA JPM 

Akizungumza wakati wa kupokea ripoti hiyo ya kwanza, Rais Magufuli alimwagia sifa Prof. Mruma kwa kumuelezea kuwa ni mzalendo wa kweli na tena ni jasiri ambaye licha ya kufuatwa fuatwa na watu mbalimbali wakiwamo viongozi ili wamhonge, kamwe hakukubali. 
Akifafanua sifa hizo za Mruma na kamati yake, Rais Magufuli alisema walikuwa jasiri hasa na kwamba, serikali ilitumia vifaa vyote vya ulinzi, lakini wapo waliojitokeza kuingilia uchunguzi huo kwa kutaka kuwarubuni wajumbe wa kamati lakini mwishowe walisimama imara na kamwe hawakutetereka. 
“Kuna mwingine anajiita profesa wakati ni dokta… alihongwa pesa na hawa watu wa makampuni ili avuruge ushahidi na kamera zikamuona, akaanza kuzungumza mambo ambayo hayajui,” alisema Rais Magufuli, akikumbushia mikikimikiki waliyoipata kina Prof. 
Mruma lakini mwishowe wakabaki kuwa imara na kukamilisha kazi waliyotumwa kwa maslahi ya taifa. 
“Wengine walidhani pesa ndiyo msaada wa kuibadilisha Kamati, nawapongeza mlimtanguliza Mungu, ” alisema Rais Magufuli wakati akipokea ripoti ya kamati ya pili kuhusu makinikia, huku akiongeza kuwa kamati hizo zilifanya kazi nzuri na zina haki ya kupewa sifa zote kwa kupigania maslahi ya Watanzania.

Advertisements
%d bloggers like this: