Skip to content
Advertisements

DC HAI GELASIUS BYAKANWA ADAIWA KUMSWEKA MWALIMU RUMANDE KWA KUSHINDWA KUTAJA JINA LA KIONGOZI HUYO.

Kwa siku za hivi karibuni wakuu wa mikoa na wilaya wamekuwa wakikemewa na wasomi, wanasheria na watetezi wa haki za binadamu kwa namna wanavyokiuka sheria kwa kuagiza watu wakamatwe na kuwekwa rumande kwa kutumia mamlaka waliyonayo.
Kwa mujibu wa sheria, viongozi hao wanauwezo wakumuweka rumande hadi saa 48 mtu au kikundi cha watu wanaotishia usalama wa eneo husika, kama hakuna njia nyingine wanayoweza kutumia kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unakuwepo.
Katika hali ya kushangaza Mkuu wa Wilaya ya Hai, Gelasius Byakanwa amemuweka mahabusu mwalimu mmoja baada ya kushindwa kujibu swali alilomuuliza.
Tukio hilo lilitokea Agosti 11 mwaka huu wakati kiongozi huyo wa wilaya akiwa katika ziara ya kutembelea shule za sekondari alipofika Shule Sekondari Lerai akiwa ameambatana na Afisa Elimu Msaidizi ambapo walifanya kikao na walimu wa shule hiyo.
Wakiwa katika kikao hicho, Byakanwa aliwauliza walimu hao kama kuna yeyote anayefahamu kwa usahihi jina lake, hakuna aliyejibu na alipowapa karatasi waandike jina lake, wote walikosea.
Baada ya muda aliwataka waalimu waandike nafasi ya shule mwaka 2015 katika mtihani wa taifa ambapo mwalimu mmoja alishindwa kuandika na alipomfuata akimwamuru aandike, mwalimu alimjibu hawezi kuandika uongo kwani hakumbuki.
Punde kidogo, DC alimfuata Mwalimu Erasto Mhanga aliyesweka mahabusu na kumtaka aeleze Halmashauri ya Wilaya ya Hai ina shule ngapi, na alijibiwa na mwalimu huyo kuwa hawezi kutaja kwa sababu hana takwimu sahihi.
Majibu hayo yalimfanya DC awapigie simu polisi wafike shuleni hapo.
Kabla gari la Polisi halijafika eneo la tukio alimwita mwalimu huyo pembeni na kumwambia achague kati ya kwenda rumande au kupiga push-up 20, lakini mwalimu alimjibu hawezi kupiga push-up kwani anamatatizo ya kiafya. Polisi walipofika shuleni hapo aliwaamuru wampeleke mwalimu huyo katika Kituo cha Polisi Bomang’ombe.
Mwalimu Mhagama aliwekwa rumande kuanzia saa 8:30 mchana hadi saa 2:00 usiku alipoachiwa huru.
Kwa upande wa Chama cha Walimu (CWT) Mkoa wa Kilimanjaro kimesema kuwa kitendo hicho cha Mkuu wa Wilaya ya Hai hakikubaliki na ni kinyume na maadili ya utumishi wa umma.
CWT imemtaka kiongozi huyo kuomba msamaha ndani ya siku 30 kuanzia Agosti 21 vinginevyo atafikishwa katika vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.
Walimu wa shule ambazo DC alipita, walilalamika kwa viongozi wa CWT kuwa waliulizwa maswali ambayo si ya kitaaluma.
Wakitaja baadhi ya maswali waliyoulizwa ni pamoja na majina ya DC, nafasi ya shule mwaka 2015, idadi ya shule Hai, magazeti ya serikali ambayo mtu kutokuyafahamu sio kosa la kupelekea kuwekwa mahabusu.
CWT imesema katu hawatalifumbia macho suala hilo na mengine kama hayo kwani ushahidi tayari wa nao na watafikisha malalamiko yao kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mama Anna Mghwira.

Advertisements
%d bloggers like this: