Skip to content
Advertisements

WAKATI Mahakama ya Juu nchini Kenya imeyafuta matokeo ya uchaguzi wa Rais uliofanyika mwezi uliopita, ikisema kuwa hayakuwa halali na kuamuru uchaguzi mpya kufanyika katika siku 60 zijazo, mambo mbalimbali yamegubika uamuzi huo. 

Mambo muhimu yaliyojitokeza na ambayo ni lazima yapatiwe ufumbuzi kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio ni kupatikana kwa majawabu ya hofu iliyoibuliwa na upande wa Muungano wa Vyama vya Upinzani (NASA) kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), haiwezi kuendesha uchaguzi wa marudio kwa uhuru na haki, huku nao upande wa serikali wa Jubilee ukihitaji majibu ya hofu kuwa Mahakama ya Juu inaendeshwa kisiasa. 
Akitoa uamuzi wa Mahakama jana, Jaji Mkuu wa Kenya, David Maraga alisema uchaguzi huo wa Rais uliofanyika Agosti 8, mwaka huu haukufanyika kwa kufuata Katiba. Katika uchaguzi huo, mgombea wa chama cha Jubilee, Uhuru Kenyatta (55) alitangazwa na IEBC kuwa mshindi katika uchaguzi huo kwa kupata kura 7,930,242 sawa na asilimia 54 dhidi ya mgombea wa NASA, Raila Odinga aliyepata kura 6,529,158 sawa na asilimia 44. 
Wagombea wengine wa Urais na kura zao ni Joseph Nyaga (36,451), Mohammed Abduba Dida (34,832), Ekuru Aukot (26,107), Shakhalaga Cyrus Jirongo (10,890) na Michael Wainanina Waura kura 8,582, zilizomweka katika nafasi ya nane. Uamuzi huo wa mahakama ni ushindi kwa upande wa upinzani, ambao uliwasilisha mahakamani kesi hiyo ya kupinga ushindi wa Rais Kenyatta. Maraga alisema uamuzi huo ulichukuliwa na majaji wanne huku wawili wakipinga. Majaji wanne walikubaliana kwamba uchaguzi huo ulikuwa na dosari. 
Hata hivyo, Majaji Njoki Ndung’u na Jackton Ojwang hawakukubaliana na wenzao. Jaji mmoja Mohammed Ibrahim hakushiriki kwenye uamuzi huo, kwani aliugua wakati kesi hiyo ikiendelea. Mawakili wa Kenyatta waliutaja uamuzi huo wa mahakama kuwa wa kisiasa na kusema hauwezi kuleta suluhisho la kudumu. Waliitaka mahakama hiyo itaje kwa uhalisia vitendo vya hujuma vilivyofanyika ili kuzuia kesi kama hiyo kurejeshwa mahakamani hapo baada ya matokeo ya uchaguzi wa marudio. 
Odinga: Safari ya Kaanani haizuiliki Akizungumza nje ya Mahakama mjini Nairobi, muda mfupi baada ya uamuzi huo, Odinga alisema kuwa jana ilikuwa ni siku ya kihistoria kwa Kenya na kwa Africa. “Kwa mara ya kwanza mahakama imefutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa urais na imetoa mfano mwema,” alisema Odinga na kuongeza; “Tulisema tangu awali kwamba safari yetu ya Canaan haiwezi kuzuiwa. Siku ya tarehe 8 Agosti tulivuka mto Jordan,” aliongeza. 
Aidha, mwanasiasa huyo alisema upinzani hauna imani kwamba Tume ya sasa ilivyo, inaweza kuandaa uchaguzi huru na wa haki. “Maofisa wengine wa tume hii wanatakiwa kuwa jela,” alisema Odinga. Kwa mujibu wa sheria za Kenya, sasa wagombea wote wanane walioshiriki kwenye uchaguzi wa kwanza, watashiriki katika raundi ya pili ya uchaguzi. Odinga, alikuwa amedai kuwa matokeo ya kura kwa njia ya elektroniki, yalidukuliwa na kuchakachuliwa kumsaidia Uhuru Kenyatta wa Jubilee kuibuka mshindi. 
Hii ni mara ya pili kwa Odinga, kupinga matokeo mahakamani, lakini mwaka 2013 alishindwa. Kenyatta awahimiza Wakenya wadumishe amani Akihutubia Taifa baada ya uamuzi huo wa mahakama, Rais Kenyatta, aliwahimiza Wakenya kudumisha amani. “Jirani yako atasalia kuwa jirani, bila kujali mrengo wake wa kisiasa, dini, rangi”. Alisema hakubaliani na uamuzi uliotolewa na Mahakama, lakini anaukubali. 
“Watu hao sita (majaji) wameamua kwamba wataenda kinyume na mapenzi ya watu. Ninyi Wakenya mlichagua wabunge wengi wa Jubilee, maseneta wengi wa Jubilee na wawakilishi wa wanawake wa Jubilee, wawakilishi wengi wa wadi wa Jubilee,” alisema. “Tuko tayari kurudi tena kwa wananchi, tukiwa na ajenda ile ile tuliyowasilisha, ajenda ya kuunganisha nchi. Kuunda chama cha taifa. Kuendeleza nchi hii. 
Hatuko kwenye vita na ndugu zetu wa upinzani.Tuko tayari kurudi kuongea na Wakenya, kuwaambia yale tunataka kutenda. “Watu wachache, watu sita, hawawezi kubadilisha nia ya Wakenya milioni 40. Wakenya ndio wataamua, na hivyo ndivyo demokrasia ilivyo,” alisema Kenyatta.” Chebukati: Waliohusika kuvuruga uchaguzi wataadhibiwa Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Wafula Chebukati amesema watu waliohusika katika kuvuruga uchaguzi, wanafaa kuwajibishwa. 
Alisema makamishna waliteuliwa miezi saba tu kabla ya uchaguzi kufanyika, lakini maofisa wengine wakuu wa tume hiyo hawakufanyiwa mabadiliko. Alidokeza kwamba, “Tume inanuia kufanya mabadiliko ya ndani” na kuangalia upya mifumo yake, kabla ya kuandaa uchaguzi mpya. Alimwalika Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kufanya uchunguzi na kufungulia mashtaka watu wote, ambao walihusika kuvuruga uchaguzi. Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2013, Uhuru alishinda kwa kura 6,173,433 sawa na asilimia 50.51 dhidi ya kura 5,340,546 za Raila, sawa na asilimia 43.7, ikiwa ni tofauti ya kura 832,887. 
Waliojiandikisha kupiga kura mwaka huo walikuwa milioni 14.3. Mabalozi waisifu Mahakama Kenya Katika hatua nyingine, Mabalozi wa nchi za Magharibi wakiwemo wa Marekani, Uingereza na Ufaransa, wameonekana kufurahishwa na uamuzi wa Mahakama ya Juu nchini Kenya. Walisema kupitia taarifa ya pamoja kuwa: “Uamuzi huru wa Mahakama hiyo umeashiria uthabiti wa demokrasia ya Kenya na kujitolea kufuata sheria. 
Watu wa Kenya wameonesha subira na imani kesi ilipokuwa inasikizwa na kuamuliwa.” Mabalozi hao walitoa wito kwa Tume ya Uchaguzi, kuanza kujiandaa kwa uchaguzi mpya wa urais na kuhakikisha utakuwa huru, wa haki, wa kuaminika, na ufanyike kwa njia ya amani. “Tuna imani katika uwezo wa Kenya na raia wake kufanya hivyo. Shughuli zote za uchaguzi zinaweza kuborehswa na tutaendelea kuunga mkono taasisi za Kenya katika kazi hii muhimu.” 
Mabalozi hao walisema demokrasia ya Kenya ni mfano wa Afrika na dunia nzima. Wananchi wagawanyika Punde tu baada ya uamuzi kusomwa, Wakenya katika baadhi ya maeneo waliandamana barabarani, kusherehekea uamuzi huo wa Mahakama. Wafuasi wa Odinga walionekana katika maeneo mbalimbali barabarani, kusherehekea maamuzi yaliyotolewa na Mahakama ya Juu nchini humo ya kufuta matokeo ya uchaguzi. Wafuasi hao walikuwa wakionesha furaha zao na kila mmoja akishangilia kwa kutumia staili yake, ambapo wapo waliokuwa wakionekana wakishangilia na matawi ya miti, huku wengine wakisikika wakiimba ‘Uhuru must go’ (Uhuru lazima ang’oke). 
Aidha wafuasi wengine walisikika wakisema kwa sasa Mahakama imetenda haki kwa uamuzi huo na imeonesha imani kwa waliokuwa wakilalamika kutotendewa haki. Pamoja na furaha iliyoonekana kwa upande wa wafuasi wa Odinga, lakini kwa upande wa wafuasi wa Kenyatta wengi walionekana kusikitishwa na uamuzi huo wa Mahakama. Akizungumza mmoja wa wafuasi wa Uhuru, alisema walikuwa wakiiamini Mahakama, lakini kwa saa hawana imani na Mahakama kwa kuwa inaonekana imeingiliwa na siasa. 
“Jubilee walipata kura nyingi hata katika wabunge ukilinganisha na vyama vingine, inakuwaje kwa Rais? Ingelikuwa mimi ndiyo Jaji ningetupilia mbali shauri hilo, lakini nashangaa uamuzi wa kufutwa kwa matokeo, kwa sababu hapo wanataka kutuhakikisha hata hao wabunge hawakupita kwa uhalali,” alisema. Wasomi, wanasiasa Dar wachambua Kufuatia Mahakama ya Juu nchini Kenya kutengua matokeo hayo ya uchaguzi, wasomi na wadau wa siasa nchini wamesema hayo ni matokeo ya kuwa na Katiba nzuri ya wananchi. 
“Maamuzi ya Mahakama ya Kenya si ushindi wa Raila, ni matokeo ya kuwa na Katiba nzuri ya wananchi inayodhihirisha kiwango kikubwa cha demokrasia na Wakenya wanapaswa kujivunia Katiba hiyo,”alisema Dk Benson Bana, Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi na Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM). Dk Bana alisema kitendo hicho, kinadhihirisha nguvu ya mihimili ya dola kufanya kazi zake kwa uhuru bila kuingiliwa na mhimili mwingine. 
“Wakenya wamedhihirisha hakuna aliye juu ya sheria na hii ni matokeo mazuri ya kuwa na Katiba nzuri na kuwa na mihimili ya dola inayofanya kazi zake wa uhuru bila kuingiliwa,Tanzania na Afrika tunapaswa kujifunza,”alisema Dk Bana. Alisema Kenya imeandika historia barani Afrika kuwa Mahakama inapaswa kuheshimiwa kwa kuwa ni chombo cha kutoa haki na kuzitana nchi na vyama vingine vya siasa, kujifunza kutafuta haki kwenye chombo hicho badala ya kuanzisha vurugu. 
Akizungumzia Katiba ya Tanzania, Dk Bana alisema ni wakati sasa wa kuanza mchakato wa kupata Katiba Mpya na hilo linawezekana kwani ana imani kuwa serikali iliyopo madarakani ni sikivu na mwaka 2020 mchakato wa kupata hiyo utakuwa moja ya agenda. “Nina imani na uongozi wa Rais John Magufuli, ingawa katika Ilani ya mwaka 2015 suala la Katiba mpya halikuwa agenda yao, ila imani yangu Rais ameliona hilo na ni kilio cha wananchi wengi hivyo, mwaka 2020 huenda Ilani ya chama chake ikaweka agenda hiyo,” alisema Dk Bana. 
Naye mwanachama wa ACT – Wazalendo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo akizungumzia hilo alisema; “Hatimaye mhimili wa Mahakama wa Kenya umedhihirisha kuwa inawezekana kuwa na Afrika yenye kuheshimu demokrasia.” Pamoja na kupongeza hatua hiyo ya Mahakama, Profesa Kitila alisema hatua hiyo ni ushindi kwa watu wote wanaopenda na kuheshimu demokrasia. 
Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe alisema uamuzi huo wa Mahakama umedhihirisha uimara, kukua kwa demokrasia na kustaarabika kwa taifa la Kenya na kuwa hilo ni somo kwa mataifa yote duniani na si Afrika pekee. Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete alisema; Niliwahi sema najifunza jambo kutoka Kenya. Leo inathibitika wakati Mahakama inafungua kurasa.”

Advertisements
%d bloggers like this: