Skip to content
Advertisements

Okwi atamba kuendelea kufunga zaidi

Mshambuliaji wa Simba na Uganda, Emmanuel Okwi.
MUDA mfupi tu baada ya kufunga bao pekee dhidi ya Misri na kuiwezesha Uganda kukaa kileleni mwa Kundi E la kufuzu Kombe la Dunia 2018, Emmanuel Okwi amesema atafunga sana msimu huu. 

Siku sita baada ya kuifungia Simba mabao manne katika ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting ya Pwani kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam katika Ligi Kuu Bara, Okwi ameifungia Uganda ‘The Cranes’ bao pekee lililoipa ushindi wa 1-0 dhidi ya Misri. 
Okwi ameifunga Misri yenye nyota kadhaa wakiwemo Mohamed Salah wa Liverpool na Mohamed Elneny wa Arsenal, ambao licha ya kupambana hawakuweza kuisaidia timu yao kusawazisha. 
Akizungumza kutoka Uganda, muda mfupi baada ya mechi dhidi ya Misri, Okwi aliliambia Championi Jumamosi kuwa, amepania kufunga mabao mengi msimu huu na atapambana kuweza kufunga muda wote. 
Akizungumza na Championi Jumamosi, Okwi amebainisha kuwa, kutokana na Mungu kuendelea kumuangazia neema ya mabao, atajitahidi kuuwasha moto katika kila mchezo atakaocheza lengo likiwa ni kulinda jina lake. 
“Naendelea kumuomba Mungu ili tu asinitupe, nataka anipe afya njema ili niweze kucheza kila mechi na kufunga mabao niwezavyo. 
“Mashabiki wengi wanatarajia kuona nafanya nini nikiwa uwanjani, ndiyo maana nasema naomba Mungu anisaidie niwe nafunga kila siku ili nilinde jina langu. 
“Kiukweli ninapokuwa kikosini hasa Simba, sipo tayari kuona timu yangu inakosa matokeo mazuri, nimekuwa nikitamani sana kufunga na kweli inakuwa hivyo, najua mashabiki wanahitaji matokeo mazuri. 
“Nasema kutoka moyoni kwamba, bado nitafunga na nitafunga kadiri ninavyopata nafasi uwanjani, Simba hii ya sasa imekamilika kila idara na sidhani kama tutakosa ubingwa msimu huu,” alisema Okwi. 
Akizungumzia mechi ya Uganda na Misri, Okwi alisema: “Ilikuwa mechi nzuri kwetu, tulipambana na kupata ushindi na itakuwa furaha kwangu nikiona tunacheza Kombe la Dunia.” 
Katika mchezo huo wa juzi ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa Mandela jijini Kampala, Uganda, Okwi alifunga bao lake dakika ya 51. 
Uganda inaongoza Kundi G ikiwa na pointi saba ikifuatiwa na Misri yenye pointi sita huku timu zote zikiwa zimecheza mechi tatu. Timu nyingine za kundi hilo ni Ghana na Congo. 
Timu hizo zitarudiana Jumanne ijayo nchini Misri.

Advertisements
%d bloggers like this: