Skip to content
Advertisements

Asha Rose Migiro arudishwa UN tena

BALOZI wa Tanzania nchini Marekani Asha-Rose Migiro

BALOZI wa Tanzania nchini Marekani Asha-Rose Migiro ni miongoni mwa wajumbe 18, walioteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, watakaounda Bodi ya Ushauri ya Masuala ya Upatanishi ya Umoja wa Mataifa. 

Bodi hiyo, iliundwa hivi karibuni baada ya Guterres kusikitishwa na matukio ya mauaji ya raia kutokana na migogoro na vita inayoendelea katika nchi mbalimbali duniani. Kutokana na hali hiyo, aliamua kuanzisha bodi hiyo ya kidiplomasia kwa ajili ya kufanya kazi ya kurejesha amani kupitia upatanisho kwenye nchi zenye migogoro. 
Bodi hiyo imejumuisha vigogo mbalimbali wanaotambulika kimataifa wenye uzoefu wa masuala ya upatanishi na diplomasia na imezingatia jinsia. Kazi kubwa ya bodi hiyo ni kumshauri Katibu Mkuu wa UN juu ya changamoto za upatanishi na kufanya jitihada mbalimbali za upatanishi katika nchi zenye migogoro. 
Pamoja na Migiro, wajumbe wengine walioteuliwa kuwemo katika bodi hiyo ni pamoja na Mwenyekiti wa Taasisi ya Graca Machel, Graca Machel, Rais Mstaafu Olusegun Obasanjo, aliyekuwa Rais wa Chile Michelle Bachelet na Mjumbe wa Baraza la Katiba Sri Lanka Radhika Coomaraswamy. 
Wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa Programu ya Usalama, Wanawake na Amani katika chuo kikuu cha Columbia Leymah Gbowee, Mjumbe wa Bodi ya Kimataifa ya Maafa Raden Mohammad Marty Natalegawa, Mjumbe wa Klabu ya Madrid Roza Otunbayeva na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Knowledge and Freedom (FOKAL) Michele Pierre-Louis. 
Pamoja na wajumbe hao, wengine ni Rais wa Taasisi ya Kimataifa ya maafa Jean-Marie Guehenno, Mjumbe wa Baraza la Wanawake viongozi Duniani Tarja Halonen, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Majadiliano ya Haki za Binadamu David Harland na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Asia Noeleen Heyzer. 
Wajumbe wengine ni Mjumbe wa Baraza la Seneti ya Jordan Nasser Judeh, Waziri Mstaafu wa Mambo ya Nje nchini Algeria Ramtane Lamamra, Rais Mstaafu wa Timor-Leste Jose Manuel Ramos-Horta, aliyekuwa Mwenyekiti wa watalaamu washauri wa UN kuhusu kujenga amani Gert Rosenthal na Askofu Mkuu wa Canterbury Justin Welby. 

Advertisements
%d bloggers like this: