Skip to content
Advertisements

Oldupai Gorge, utafiti wabainisha huenda ni sehemu iliyokuwa bustani ya Edeni         

KWA UFUPI

Eneo hilo linalotajwa kuwa la ajabu lipo ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, takriban kilomita 150 kutoka Arusha mjini na takriban kilomita 800 kutoka jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu mstaafu wa Israel Ehud Barak na familia yake walikuja nchini kutalii na moja ya maeneo waliyofika ni Oldupai Gorge, sehemu inapopatikana historia muhimu ya binadamu.
Eneo hilo linalotajwa kuwa la ajabu lipo ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, takriban kilomita 150 kutoka Arusha mjini na takriban kilomita 800 kutoka jijini Dar es Salaam.
Baada ya kutembelea eneo hilo, Barak alitoa kauli moja tu: “Hapa ni eneo muhimu sana duniani kwani ndiyo makutano ya historia ya binadamu.”
Barak alikuwa Waziri Mkuu wa Israel mwaka 1999 hadi 2001, akiwa kiongozi wa Chama Labor hadi mwaka 2011 na pia aliwahi kuwa Waziri wa Ulinzi wa Israel kuanzia 2007 hadi 2013.
Wakati Waziri Mkuu huyo wa zamani na familia yake wanafunga safari kuja nchini katika eneo la Oldupai umbali wa takriban kilomita 6,000, Watanzania ambao wanaishi kilomita chini ya 200 tu hawajawahi kufika eneo hili.
Takriban saa tano nimekuwa katika eneo hili nashuhudia idadi kubwa ya watalii kutoka nje ya Tanzania wengi wakiwa na familia zao, wakifika hapa kupata historia ya eneo hili, lakini Watanzania ninao waona ni madereva wa magari yaliyoleta watalii na wafanyakazi wa eneo hili.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Lamo Makani anasema eneo la Oldupai ni eneo muhimu sana katika historia ya mwanadamu.
Makani anasema eneo hili, pamoja na eneo la jirani la Laitole ambalo zipo alama za nyayo zenye zaidi ya miaka milioni 3.6 za zamadamu linapaswa kulinufaisha Taifa.
“Ni ukweli uliowazi kuwa bado hatujalitumia vizuri sana eneo hili kuvuta mamilioni ya watalii duniani na Watanzania, lakini kama wizara tunaendelea kuhakikisha eneo hilo ambalo Mungu ametujalia linatunufaisha” anasema.
 
Kuna nini Oldupai?
Mhifadhi wa malikale katika bonde la Oldupai, John Paresso anasema eneo hili ni chimbuko la historia ya zamadamu na kuna ushahidi wa zaidi ya miaka milioni mbili iliyopita.
Anasema jina halisi la eneo hilo ni Oldupai na siyo Olduvai kama ambavyo lilielezwa na mmoja wa watafiti wa mwanzo wa eneo hili, Profesa Wilhalm Katt Windle ambaye alishindwa kutamka vyema neno la Kimasai Oldupai na kusema Olduvai.
Paresso anasema Oldupai ni jina la kimasai ambalo lina maana ya katani ambazo zinapatikana katika bonde hilo.
Katani hizo ni nyembamba tofauti na katani za kawaida na zinahimili hali ya joto na ukame katika eneo hilo.
Anasema katika bonde hili, kuna mabaki mbalimbali za damadamu wa kale na wanyama ambao hivi sasa hawapo tena duniani ambao waliishi zaidi ya miaka milioni mbili iliyopita.
Miongoni mwa wanyama hao ni tembo wa kale, nyati wa kale ambao walikuwa na pembe ndefu zaidi ya ng’ombe, farasi wa kale, swala na twiga wa kale ambao walikuwa na pembe ndefu.
Katika eneo hili pia kuna mabaki mbalimbali ya zamadamu walioishi miaka zaidi ya millioni mbili iliyopita, kuna mawe ambayo yalitumika kwa shughuli zao mbalimbali na zana nyingine.
Katika bonde hili pia kuna matabaka sita ya udogo na tafiti zimefanyika kuanzia miaka milioni mbili iliyopita hadi miaka 100 iliyopita.
Anasema tafiti nyingi ambazo zinaendelea katika bonde hilo zinafanywa katika matabaka hayo sita na imegundulika kuna mabaki ya zamadamu wa kale, visukuku na wanyama mbalimbali wa kale.
Katika matabaka hayo, takala la sita lenye miaka zaidi ya milioni mbili iliyopita, yaliguliwa mabaki ya zamadamu wa kale (Australepithe cus boisei).
Tabaka la pili lenye umri wa zaidi ya miaka milioni 1.9 yalipatikana mabaki ya zamadamu aliyekuwa anatumia mikono (Homo habilis na Zinjanthoopus).
Paresso anasema tabaka la tatu yalipatikana mabaki ya zamadamu (Homoerectus) ambaye alikuwa anatembea miaka kati ya milioni 1.5 hadi 500,000.
Anasema watafiti katika tabaka la nne ambalo lina miaka kati ya 400,000 hadi 200,000 iliyopita walikuta mabaki ya zamadamu Homo Ectus ambaye alikuwa anatumia mikono, sawa na tabaka la miaka 100,000 hadi 10,000 iliyopita.
“Katika maeneo haya pia kuna mabaki ya wanyama wa kale ambao wengi hawapo hivi sasa hali ambayo inaonyesha umuhimu wake,” anasema.
Mhifadhi Msaidizi katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Orgoo Mauyai anasema utajiri wa historia katika eneo la bonde la Oldupai ni mkubwa na bado utafiti unaendelea.
“Hadi sasa bado kuna watafiti wanaendelea kugundua vitu mbalimbali katika bonde hili hadi maeneo la Laetoli na tunaimani mengi yatagundulika na hivyo kuvutia mamilioni ya watalii,”anasema.
 
Ugunduzi unaoendelea
Licha ya utafiti katika bonde hili ulioanza tangu mwaka 1913 uliofanywa na Wajerumani na baadaye utafiti wa Dk louis Leakey na mkewe Mary, waliopata visukuku 60 vya zamadamu bado hadi sasa utafiti unaendelea na umekuwa na mafanikio makubwa.
Hivi karibuni watafiti wa mambo ya kale na wanasayansi kutoka mataifa ya Ulaya, Amerika na Afrika, wamegundua masalia 19 zaidi ya visukuku vya zamadamu katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro na hivyo kuanza kuamini kuwa bustani ya Edeni ilikuwa Ukanda wa bonde la Ufa wa Ngorongoro, Kenya na Ethiopia.
Vitabu vitakatifu vinaitajwa bustani ya Eden kuwa ni eneo ambalo binadamu wa kwanza Adamu na Eva (Hawa) waliishi kabla ya Mungu kuwatoa baada ya kumuasi.
Profesa Phidelis Masao wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Mambo ya Kale anasema katika eneo la bonde la Oldupai Gorge, watafiti hao, walipata masalia hayo ya visukuku vya zamadamu 19 yanafanya eneo la Ngorongoro pekee kupatikana masalia 79.
Profesa Masao anasema ugunduzi mpya unaoendelea katika eneo la Oldupai na Laetoli unathibitisha huenda binaadamu wa kwanza waliishi katika mabonde hayo.
“Ugunduzi huo, sambamba na unaoendelea katika maeneo ya Turkana nchini Kenya na Afaa nchini Ethiopia unaonyesha kuwa eneo la bonde la ufa kutoka Tanzania, Kenya na Ethiopia ndiyo ilikuwa bustani ya Edeni,” Profesa Masao.
Naye, Profesa Robert Blumeuschine kutoka taasisi ya utafiti wa mambo ya kale ya Past ya nchini Afrika ya kusini anasema eneo la Ngorongoro ni muhimu kwa sasa kwa historia ya dunia.
Profesa Blumeuschine anasema watafiti wote wakubwa duniani wataendelea kufika Ngorongoro ili kujua vitu vingi kuhusiana na historia ya mwanadamu.
Katika eneo hilo la Laetoli karibuni pia yamegundulika mabaki ya zamadamu wanadaiwa kuishi miaka milioni 3.7 iliyopita.
 Ugunduzi huu ni wa pili mkubwa kufanyika baada ya ule wa Dk Mary Leaky na wenzake uliofanywa mwaka 1978 katika eneo hilo.
 
Mikakati ya boresha Oldupai
Kutokana na umuhimu wa eneo hili la Oldupai na mengine ambayo sasa yanatambulika kama maene ya utalii wa kijiolojia (Geopark), Jumuiya ya Ulaya (EU) tayari imetoa kiasi cha Sh4.2 bilioni kuboresha maeneo haya.
 Meneja wa Idara ya Urithi wa Utamaduni wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Mhandisi Joseph Mwankunde anasema fedha hizo, zimetolewa kuboresha mradi wa maeneo muhimu kijiorojia katika hifadhi hiyo ambayo ni urithi wa utamaduni na vivutio cha watalii.
 Anasema fedha hizo zitatumika katika uboreshaji na ujenzi wa jengo la makumbusho la oldupai, majengo ya kuuzwa bidhaa za asili, njia za kutembelea watalii katika eneo la ziwa Natron, mazingira ya Mlima Oldonyolengai na maeneo ya Creta ya Ngorongoro na Laitole.
 Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro, Dk Fred Manongi anasema mamlaka hiyo imejipanga kuongeza idadi ya watalii katika hifadhi hiyo kupitia Bonde la Oldupai na maeneo mengine ya vivutio.
Anasema kwa sasa watalii wanaotembelea hifadhi ni kati ya 700,000 hadi 800,000 kwa mwaka idadi ambayo ni ndogo kulinganisha na watalii wanaopaswa kuja nchini hasa kutokana na vivutio muhimu vilivyopo Ngorongoro.
“Tunataka kuendeleza eneo hilo la utalii ya kijilojia kwani ndiyo utalii mpya ambao unapendwa na nchi za Asia kama China na tunatarajia kuongeza watalii wa ndani na nje kuja Oldupai na maeneo mengine kuona urithi hii,” anasema.

Advertisements
%d bloggers like this: