Skip to content
Advertisements

UMRI GANI NI SAHIHI KUOLEWA? SOMA HAPA!

Kwa tuliokuwa pamoja wiki iliyopita tulijifunza juu ya heshima husasan kwa wanawake. Niliwaelekeza kuhusu umuhimu wa kuwatii waume zao maana si maneno ya yangu ni mpango wa Mungu na ndiyo maana tukaletewa kwenye maandiko matakatifu.

Mwanaume na mwanamke kila mmoja ana wajibu wake katika kutekeleza mpango wa Mungu. Nakumbuka nilikuachia maandiko haya:

“Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo.

“Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno.”-Waefeso 5:21-25.

Bila shaka kwa waliokuwa tayari kujifunza, walijifunza vitu vingi kutokana na mada hiyo nina hakika wengi mtakuwa kwa namna moja au nyingine, mmebadilika.

Turudi katika mada ya leo. Linapokuja suala la ndoa, wapo watu wamekuwa wakijiita wao ni fungu la kukosa. Wanalalamika kwamba hawana bahati ya kuolewa. Wanahangaika huku na huko kutafuta wenza wao wa maisha.

Kutokana na kukutana na mitihani mbalimbali, wanajikuta wamepoteza uelekeo. Inafika wakati wanakuwa wasumbufu. Kwa mwanamke, kila mwanaume anayekutana naye anafikiri ndiye mume sahihi. Anafikiri anaweza kumshawishi awe mume, kamwe akili yake haiwazi mawazo hasi kwa huyo mwanaume.

Hawazi kwamba pengine huyo mwanaume si muoaji. Hana sifa ya kuwa mume. Pengine ni malaya wa kupindukia. Hafikirii kabisa kwamba pengine huyo mwanaume ana mke wake. Anachoangalia yeye kutafuta nafasi yake ili aweze kummiliki mwanaume huyo.

Matokeo yake sasa, anaweza kujikuta ameingia kwenye mikono ambayo si salama. Mwanaume anaweza kumridhisha kwa sababu ya usumbufu wake. Akakubali kushiriki naye tendo kisha kumuacha hewani. Yeye analazimisha penzi, mwenzake anamfanya kama tairi la spea.

Kwa wanaume pia wapo wa aina hiyo. Wanafikia hatua ya kuhaha pindi waonapo umri unakwenda na wao bado hawajaingia kwenye ndoa. Ndio pale sasa mwanaume, kila mwanamke anayekutana naye anafikiri ndiye mkewe.

Kila mwanamke anamtongoza. Anamtaka awe mke bila kujua, anayemtongoza hana sifa ya kuwa mke. Pengine si mwaminifu. Hana tabia njema. Au pengine tayari ameolewa na mtu mwingine. Unalazimisha kuoa mtu ambaye tayari ana mume, unategemea nini?

Utajibiwa kistaarabu, ukilazimisha utajibiwa vibaya. Unapata fedheha na kujiona kama huna bahati. Kumbe pengine ungeheshimu majibu na kukubali uhalisia kwamba mwenzako ameshapata mwenza, usingefikia hatua ya kujidhalilisha.

Suala la msingi hapa kutambua ni kwamba, kuolewa au kuoa ni sauala linalotokana na muda muafaka. Kwamba kuna muda ukifika hata iweje, utaolewa au kuoa. Hakuna kanuni maalum kwamba unapaswa kuolewa au kuoa ukiwa na umri gani.

Wapo walioolewa wakiwa na umri mkubwa sana, wapo walioolewa wakiwa na umri mdogo sana. Wote wanafurahia au wanahuzunikia maisha ya ndoa. Kama ni furaha ya ndoa, wote wanaipata na kama ni machungu ya ndoa, wote wanayapata kulingana na wakati.

Kuna kitu kinaitwa bahati. Kila mtu ana yake, hakuna sababu ya kulazimisha. Kama ipoipo tu. Vuta subira, muombe Mungu akupe mke au mume mwema na muda wako utafika. Ishi kwa matumaini kwamba utampata wako wa maisha.

Tengeneza mazingira rafiki ya kuingia kwenye maisha ya ndoa. Jiheshimu, muda wako utafika na wewe utapaswa kuheshimu ndoa yako pindi itakapotokea.

Advertisements
%d bloggers like this: