Skip to content
Advertisements

MPINZANI WA KAGAME, DIANE RWIGARA, AFIKISHWA MAHAKAMANI RWANDA

Mwanasiasa wa upinzani nchini Rwanda, Diane Rwigara akiingia mahakamani.

MWANASIASA wa upinzani nchini Rwanda, Diane Rwigara, mama yake na dada yake, wamefikishwa mahakamani mjini Kigali kwa mara ya kwanza, wiki mbili baada ya kukamatwa na polisi.
Watatu hao wameshitakiwa kwa kuchochea uasi nchini, mashtaka waliyoyakanusha wakisema yana misingi ya kisiasa.

Diane Rwigara alizuiwa kugombea kiti cha urais katika uchaguzi uliofanyika mwezi Agosti mwaka huu ambapo Rais Paul Kagame alishinda kwa asilimia 98 ya kura.

Mwandishi wa BBC, Yves Bucyana, mjini Kigali amesema chumba cha mahakama kilikuwa kimejaa watu wengi miongoni mwao wakiwemo wanadiplomasia wa baadhi ya nchi za Magharibi na Marekani.

Ulinzi ukiwa umeimarishwa, watuhumiwa hao watatu waliingizwa mmoja baada ya mwingine katika chumba cha mahakama wakiwa wamefungwa pingu.

Jaji alifungua kikao kwa kusikiliza hoja ya watuhumiwa, Diane Rwigara na mama yake, Adeline Rwigara, ambapo washitakiwa wamesema wanataka kuwasiliana na mawakili wao. Wamesema wamewasiliana mara moja tu kabla ya mawakili hao kukataliwa kuwaona tena ambapo dada yake, Anne Rwigara, akisema hajapata kabisa wakili.

Wote wameomba kesi iahirishwe ili kupata muda zaidi wa kutayarisha kesi dhidi yao.

Hoja hiyo imekubaliwa kwa kesi kuahirishwa hadi Jumatatu wiki ijayo.

Mashitaka yanayowakabili yalikuwa tayari yamewekwa hadharani na mwendesha mashtaka kabla ya wao kufikishwa mahakamani leo. Wote watatu wameshitakiwa kwa kuchochea uasi miongoni mwa wananchi.

Zaidi ya hayo, Diane Rwigara ameshtakiwa kwa kughushi nyaraka huku mama yake, Adeilne Rwigara, akishtakiwa pia kwa kosa la kuwagawa wananchi kwa misingi ya kikabila. Awali walipokuwa katika ngazi ya upelelezi wa mwanzo walishitakiwa kwa makosa ya kutaka kuiangusha serikali.

Wote wamepinga mashitaka dhidi yao wakisema yana misingi ya kisiasa. Diane Rwigara mwenye umri wa miaka 35 alizuiwa kugombea kiti cha urais uliofanyika mwezi Agosti mwaka huu.

Tume ya uchaguzi ya Rwanda ilisema alifanya ulaghai katika kutafuta saini za wafuasi wake ili kutimiza matakwa ya tume hiyo. Tangu ulipoanza mchakato huo wa kutaka kuingia ikulu, Diane Rwigara amejitokeza kama mpinzani na mkosoaji mkuu wa chama tawala RPF.

Baada ya kukataliwa kugombea urais alianzisha vuguvugu alilotaja kuwa na lengo la kupinga uonevu na kupigania haki miongoni mwa wananchi.

Advertisements
%d bloggers like this: