Skip to content
Advertisements

Mawaziri kuanika mikakati yao leo

WAKATI leo Rais John Magufuli akitarajiwa kuwaapisha mawaziri na manaibu mawaziri wapya, aliowateua mwishoni mwa wiki, kwa sasa macho na masikio ya Watanzania yameelekezwa kwenye wizara iliyokuwa moja na kugawanywa ya Nishati na Madini kutokana na wizara hizo hivi karibuni kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo wizi wa rasilimali za madini ya dhahabu na tanzanite. 

Aidha, wengi wa mawaziri hao wamebainisha kuwa wataanika mikakati yao ya utendaji kwenye wizara walizoteuliwa baada ya kuapishwa Ikulu jijini Dar es Salaam leo. Katika uteuzi wake, Dk Magufuli aliigawa Wizara ya Nishati na Madini na kuzifanya wizara mbili tofauti na kila moja akiipa waziri wake, kitendo kilichopokelewa na kuungwa mkono na wengi kutokana na unyeti wa wizara hizo. 
Akizungumza kwa njia ya simu jana na gazeti hili kuhusu maoni na mikakati yake mara baada ya kuteuliwa kuongoza wizara hiyo nyeti, Waziri wa Madini, Angela Kairuki alisema atazungumza leo mara baada ya kuapishwa. Waziri Kairuki anaingia katika historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kukabidhiwa wizara hiyo, ambayo imekuwa ikitajwa kuwa yenye changamoto nyingi kuliko wizara nyingine yoyote huku mawaziri wengi waliopita katika wizara hiyo wakipatwa na misukosuko. 
Kabla ya uteuzi wake, Kairuki alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), moja ya wizara nyeti nyingine, lakini mwanamama huyo ameimudu na usimamizi wake mzuri ndani ya wizara hiyo unatajwa kama moja ya sifa za msomi huyo wa sheria kupewa kuongoza Madini. 
Baada ya mgawanyo huo, Wizara ya Nishati kwa sasa inashikiliwa na Dk Medard Kalemani ambaye awali alikuwa ni Naibu Waziri wa wizara hiyo chini ya Profesa Sospeter Muhongo, ambaye alifutwa kazi kutokana na kashfa ya usafirishaji nje makinikia. Kugawanywa kwa wizara hiyo, kumepokelewa kwa mikono miwili kutokana na ukweli kuwa wizara hiyo pamoja na kukabiliwa na changamoto, mawaziri wake wamekuwa wakikumbwa na misukosuko kwa muda mrefu. 
Katika Serikali ya Awamu ya Tano pekee, tayari mawaziri wawili wameachia ngazi kutokana na kashfa mbalimbali zinazohusu mikataba ya madini akiwemo Profesa Muhongo na aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene. Pia aliyekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani alijiuzulu kutokana na mikataba inayohusu madini. 
Hivi karibuni, Spika wa Bunge Job Ndugai aliishauri serikali kuangalia uwezekano wa kuitenganisha Wizara ya Nishati na Madini ili ifanye kazi zake kwa umakini na kupunguza matatizo ambayo yamekuwa yakijitokeza katika sekta ya madini. Spika Ndugai alisema wizara hiyo imekuwa ikikabiliwa na mzigo mkubwa wa kusimamia masuala yanayohusu madini na nishati, hivyo kusababisha usimamizi mbovu hasa katika sekta ya madini. 
Alitoa ushauri huo Ikulu hivi karibuni, baada ya kukabidhiwa ripoti za kamati mbili alizoziunda kwa ajili ya kuchunguza biashara ya madini ya almasi na tanzanite Naye Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe wakati akitoa maoni yake kuhusu mabadiliko ya baraza jipya la mawaziri, alimpongeza Dk Magufuli kwa kuona umuhimu wa kutenganisha wizara hiyo ya nishati na madini. 
Kiongozi huyo alikaririwa na gazeti moja jana akisema kwa miaka saba, Kambi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikiomba kugawanywa kwa wizara hiyo ya Nishati na Madini kutokana na kuwa na majukumu mengi na ni nyeti. Naye Waziri mteule, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika alisema amejipanga kuzungumza leo kuhusu uteuzi wake huo mara baada ya kuapishwa. “Naomba unisubiri, nitaongea vizuri kuhusu hayo yote kesho, mara baada ya kuapishwa,” alisisitiza Mkuchika (69) alipopigiwa simu na gazeti hili. 
Mbunge huyo wa Newala aliwahi kusimamia Utawala Bora akiwa katika Serikali ya Awamu ya Nne. Naye Naibu Waziri Mteule wa Maji na Umwagiliaji ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Pangani (CCM), Jumaa Awesso alimshukuru Rais Magufuli kwa kumteua katika nafasi hiyo ambayo hakuitarajia na kuahidi kufanya kazi kwa kasi na pia kuhakikisha Watanzania kwa ujumla wanaondokana na kero ya maji ikiwamo wilaya yake ya Pangani. Aliyasema hayo mara tu baada ya kuteuliwa katika nafasi hiyo katika mahojiano maalumu na gazeti hili. 
“Kwa kweli namshukuru Mheshimiwa Rais kuniteua kwani sikutarajia, nilivyoambiwa na baba yangu mdogo, Hussein Aweso kuwa nimeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji sikuamini mpaka nilivyoona marudio kwenye televisheni ndiyo nikaamini,” alieleza Aweso. Aliongeza kuwa kutokana na uteuzi huo, wilaya ya Pangani imepewa heshima kubwa kwani ni mara ya kwanza kuwa na waziri. 
“Hii ni heshima kubwa kwa Pangani kuwa na waziri kwani tangu iwe wilaya haijawahi kupata waziri tangu awamu ya kwanza ya uongozi, na changamoto kubwa tuliyokuwa nayo ni maji licha ya kuwa na chanzo kikuu cha maji cha mto Pangani na ninaahidi kuwa nina deni kwa wakazi wa jimbo hili,” alieleza mbunge huyo kijana. 
Kwa upande wake, Mbunge wa Nzega Vijijini ambaye pia alikuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto kabla ya uteuzi mpya wa Wizara ya Maliasili na Utalii hiyo, Dk Hamisi Kigwangalla aliwataka Watanzania kuendelea kumuombea dua pamoja na ushirikiano katika majukumu yake mpya. 
“Nimepokea salamu nyingi za pongezi na shukrani kwa Mungu aliye juu. Sintoweza kumjibu kila mtu, uungwana ni kutambua pongezi zenu na dua tele mlizotuombea, nawashukuru sana ndugu zangu. Tuzidi kuombeana dua tu. “Tuna kazi ngumu ya kukimbia kukidhi matarajio ya kiongozi wetu Mkuu aliyetuamini na matarajio ya wananchi wenzetu. 
Binafsi nawaahidi nyote kuwa sintowaangusha! Ahsanteni sana ndugu zangu, natarajia ushirikiano wenu wa kila hali,” alieleza Dk Kigwangalla. Awali taarifa za kuteuliwa kwake katika wizara nyingine, alizipata kupitia kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi kwa njia ya simu wakati akiwa kwenye majukumu ya ziara ya kuboresha mfumo wa afya wilayani Nachingwea, Kata ya Kilimalondo umbali wa zaidi ya kilometa 100, kutoka Makao makuu ya wilaya. 
Alisitisha ziara yake hiyo ambayo alitakiwa kuendelea katika vijiji na wilaya nyingine ya Liwale. Dk Magufuli alifanya mabadiliko katika Baraza lake la Mawaziri kwa kuwahamisha baadhi yao kwenda wizara nyingine, kuwapandisha baadhi ya manaibu waziri kuwa mawaziri kamili, kuwaingiza wapya na kuwaacha baadhi yao nje ya Baraza hilo. Mabadiliko hayo aliyoyafanya juzi Ikulu jijini Dar es Salaam, pia yameongeza wizara kutoka 19 za awali kwa kuzigawanya baadhi ya wizara hizo na kufanya jumla ya wizara zote kuwa 21. Mawaziri wote wanaostahili kuapishwa kulingana na mabadiliko hayo wanaapishwa leo ikulu Dar es Salaam. 
Source: Habari Leo

Advertisements
%d bloggers like this: