Skip to content
Advertisements

Kuharakisha kumpeleka shule mtoto kunaweza kumdumaza

Mwanzoni mwaka huu, niliamua kumpeleka mwanangu wa miaka mitatu shuleni.
Katika umri huo mdogo, kwa kweli tulitamani mtoto angebaki nyumbani. Lakini kwa kuwa mimi na mke wangu tunalazimika kwenda kazini asubuhi, tuliona ni vyema mtoto akapata mahali salama pa uangalizi.
Hata hivyo, hatukutarajia mtoto mdogo kiasi hicho akajifunze kusoma, kuandika wala kuhesabu. Tuliichukulia shule kama sehemu salama zaidi ya malezi kwa mtoto kuliko kumwacha nyumbani na msichana wa kazi.
Kutofurahia shule
Siku chache baada ya mtoto kuanza kuhudhuria shule, tulianza kuona mabadiliko. Kwanza, mtoto alirudi nyumbani akiwa amechoka na hivyo alilala mapema zaidi kuliko ilivyokuwa kawaida yake. Hatukupata wasiwasi kwa sababu usingizi wa kutosha ni mojawapo ya mahitaji muhimu kwa afya ya mtoto.
Tulianza kupata wasiwasi mtoto alipoonekana kukosa shauku ya kwenda shule. Kama wazazi tulifikiri shule ni mahali pa furaha zaidi kwake hasa kwa sababu anakutana na wenzake wa umri wake.
Kingine tulifikiri kwa sababu shuleni angepata muda wa kucheza michezo mingi isiyopatikana katika mazingira ya nyumbani, hivyo kwa vyovyote angekuwa na msisimko wa kwenda.
Kwa hiyo hali hiyo isiyotarajiwa ya mtoto kutofurahia shule ilitustua kidogo kama wazazi hasa kwa sababu wakati mwingine aligoma kabisa. Fahari ya kuvaa nguo za shule, kubeba begi kama dada yake haikutosha kumpa sababu ya kutamani kwenda shule. Wakati mwingine ilibidi kufanya kazi ya ziada kumshawishi.
Mzigo wa masomo
Niliamua kufanya uchunguzi mdogo kubaini kitu gani hasa kilisababisha yote hayo. Nikagundua mambo kadhaa. Kwanza, ugeni wa mazingira. Kama ambavyo baadhi ya sisi watu wazima huhitaji muda kuzoea mazingira mageni, ndivyo inavyotokea kwa watoto wadogo.
Kitendo cha kuondoka nyumbani, mahali anapopachukulia kuwa salama zaidi kwake, na kwenda kukaa saa nyingi mahali pengine akiwa na watu asiowafahamu vizuri, kinaweza kumfanya asifurahie. Hata hivyo, nilitarajia angezoea mazingira yale baada ya muda kwa sababu si tu walezi wake shuleni walikuwa wachangamfu kwa watoto, lakini pia wingi wa watoto wa umri wake sambamba na upatikanaji wa vifaa vya michezo, ungemsaidia kufurahia vitu vingi zaidi kuliko kama angebaki nyumbani.
Baadaye nikagundua utaratibu wa malezi katika kituo hicho ulikuwa na kasoro. Watoto wale wadogo walifundishwa masomo ambayo, kwa hali ya kawaida, hufundishwa kwa watoto wa darasa la kwanza wenye miaka kati ya sita na saba.
Mtoto wa miaka mitatu, kama huyu wa kwangu, alilazimika kuanza kujifunza ‘alfabeti’, ‘tarakimu za Hisabati’ na hata kuanza kukariri baadhi ya maneno kwa lugha ya Kiingereza. Malezi yalitilia mkazo zaidi kwenye taaluma kuliko michezo.
Matarajio ya sisi wazazi
Nilimuuliza mkuu wa kituo hicho kujua mtazamo wake kuhusu jambo hilo. Akajibu:, ‘Hapa tunawaandaa vizuri ili watakapokwenda darasa la awali wasipate shida. Kwa hiyo tunahakikisha wanapotoka hapa wawe wanajua kusoma, kuandika na kuhesabu. Vilevile, tunawafundisha lugha ya Kiingereza ambayo ni muhimu kwa masomo ya darasa la kwanza.’
Mwalimu huyu, kwa jinsi alivyoongea, alionekana kuamini kuwa msisitizo mkubwa kwenye masomo una manufaa kwa watoto kwa sababu uliwaandaa kufanya vizuri katika ngazi za juu. Nikataka kujua kwa nini wasingesubiri watoto wafike ngazi husika ili wajifunze kile wanachotarajiwa kujifunza.
Hakunificha sababu, kwani alisema: ‘Nyinyi wazazi ndio wateja wetu na hicho ndicho mnachotaka. Ukimleta mtoto wako hapa, unatarajia ajue kuongea Kiingereza, asome na aweze kuandika na kufanya hesabu. Vyote hivyo ndani ya muda mfupi.’
Nikakumbuka wakati ninatafuta nafasi ya darasa la kwanza kwa binti yangu wa kwanza. Haikuwa kazi rahisi. Watoto wanaotarajia kuanza darasa la kwanza ilibidi wafanye mtihani wa kupima uwezo wao wa kusoma, kuandika kwa Kiingereza na walipaswa kuwa na uwezo wa kufanya mahesabu.
Kimsingi, walimu wa darasa la kwanza waliopaswa kuwa na kazi ya kufundisha mambo hayo matatu, nao walitarajia kuletewa watoto ambao tayari wameshajifunza yale wanayopaswa kuwafundisha baada ya kuwapokea shuleni.
Kwa hiyo nikaona mwalimu alikuwa sahihi. Matarajio makubwa ya wazazi yanachochea jitihada kubwa za walimu kukidhi matarajio hayo. Kwa bahati mbaya hali kama hiyo inachangia kumlazimisha mtoto mdogo wa miaka miwili au mitatu kujifunza mambo ambayo wakati mwingine hayalingani na umri wake.
Makuzi yanayosahaulika
Nikirudi kwa mtoto wangu huyu wa miaka mitatu, mara nyingi alirudi nyumbani akiwa na ‘kazi nyingi za nyumbani.’ Walezi wake shuleni walifanya hivyo kwa nia njema ya kuturidhisha sisi wazazi walioamini tunataka kuona matokeo mazuri ya fedha tunazolipa kama ada ya ‘masomo.’
Kazi hizi, pamoja na nia njema ya waliozitoa, zilikuwa na mchango mkubwa katika kumchosha akili. Kazi hizi kwa kweli hazikuzingatia uwezo wa mtoto. Katika umri wake wa miaka mitatu, shughuli ya maana anayoihitaji zaidi ingekuwa michezo.
Kupitia kucheza, mtoto angejifunza mambo ambayo yangekuwa msingi wa maisha yake kuliko kukazaniwa kushika masomo. Michezo, mathalani, ingemfundisha umuhimu wa kushirikiana na wenzake, kuelewa wenzake wanafikiri nini, kuchangamsha ufahamu wake na kwa ujumla, kufurahia utoto wake.
Lakini kwa sababu ya ‘fikra za maendeleo’ watoto hawa wamenyimwa fursa ya kuuishi utoto wao na badala yake wanakabiliwa na shinikizo la kufanikiwa kupitia ‘ufaulu.’
Sisi wazazi wenye ‘fikra za kimaendeleo’ kwa kweli hatutarajii mtoto acheze, akosee, afeli, ajifunze. Kilicho muhimu kwetu ni mtoto ‘kushika masomo’ na kujua Kiingereza.
Matokeo yake watoto wanajikuta wakitumia muda mwingi kwenye kazi ambazo wakati mwingine zinawazidi umri. Haya yote yanafanywa kwa gharama ya maeneo mengine muhimu ya ukuaji wa mtoto.
Kwa kuwa nilishaanza kuona matokeo ya mtazamo huo wa kumharakisha mno ‘masomo’ mwanangu, nilimwambia mwalimu nimempeleka mwanangu pale ili apate nafasi ya kucheza. Mwalimu alinishangaa.Itaendelea

Advertisements
%d bloggers like this: