Skip to content
Advertisements

Uingereza ; Mwanasheria aenda mahakamani kumtetea shetani

Giovanni Di Stefano

Mwanasheria nguli na Wakili wa Mahakama kuu nchini Uingereza Giovanni Di Stefano ameweka kusudio la kufungua shauri kwenye mahakama ya haki ya umoja wa Ulaya (The Court of Justice of the European Union) kuzuia watu kumtuhumu na kumsingizia shetani mambo mbalimbali bila kuwa na ushahidi.
Wakili huyo amesema kwa muda mrefu sasa shetani amekuwa akituhumiwa kwa mambo mbalimbali bila kupewa nafasi ya kusikilizwa. “Mara nyingi watu wanapofanya mambo mabaya katika jamii hawataki kuwajibika na hivyo kumsingizia shetani, na hivyo shetani huhukumiwa bila kupewa nafasi ya kusikilizwa” Giovanni ameliambia gazeti la The Express la nchini humo.
Ikiwa shauri hilo litakubaliwa, mahakama inaweza kuweka zuio la kutumia jina la shetani kwa mambo mabaya bila uthibitisho usiotilia shaka kwamba kweli shetani amehusika na matukio hayo. Wakili Giovanni anasema kwa siku za karibuni watu wengi wamekuwa wakifanya makosa lakini wakijitetea kuwa wamepitiwa na shetani jambo ambalo linatilia mashaka ukweli wake.
Giovanni anataka mtu yeyote atakayesema amepitiwa na shetani aweze kuthibitisha mbele ya mahakama pasi na shaka yoyote kuwa kweli shetani alimpitia.
Wakili huyu mwenye vituko vingi, amewahi pia kusema ikiwa atapewa nafasi ya kuzungumza na Mungu basi atamuomba nafasi ya kumtetea shetani siku ya kiyama.
Hata hivyo wakili mkongwe mwanamama Emma Jones wa kampuni ya Leigh Day Attorneys amesema anategemea shauri hilo kutupiliwa mbali na Mahakama kwani halina msingi wowowte wa kisheria.

Advertisements
%d bloggers like this: