Skip to content
Advertisements

Swahiba amwacha solemba Lowassa

Simba ambaye aliwahi pia kushikilia nafasi kadhaa za uwaziri katika utawala wa serikali ya awamu ya nne, alikuwa akimuunga mkono Lowassa bila kificho katika harakati zake za kutimiza ndoto ya ‘safari ya matumaini’ kuelekea Ikulu, wakati huo akiwa miongoni mwa watangaza nia ya kugombea urais kwa tiketi ya CCM kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

Hata hivyo, jina la Lowassa ni miongoni mwa yale yaliyokatwa mapema katika mchakato huo huku Simba akipinga uamuzi uliofanywa na Kamati Kuu ya CCM ambayo yeye alikuwa mmoja wa wajumbe wake, chanzo kikiwa ni kuondoshwa kwa Lowassa.
Jina la Rais John Magufuli ndilo lililoibuka kidedea hatimaye, huku Lowassa akitangaza kuhama chama hicho na kujiunga Chadema ambako mwishowe aligombea urais kwa tiketi ya chama hicho na vingine vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Simba hakuwa miongoni mwa vigogo kadhaa wa CCM waliomfuata Lowassa katika ‘safari ya matumaini’ nje ya CCM. Machi, mwaka huu, Simba alijikuta akitimuliwa uanachama wa CCM baada ya kukutwa na hatia ya kuwa miongoni mwa wale waliokuwa wakikisaliti chama hicho wakati wa harakati za kuchuana na Ukawa katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015 na Magufuli kuibuka na ushindi wa asilimia zaidi ya 58. Lowassa alipata asilimia takribani 40 ya kura halali zilizopigwa.
Baada ya Simba kufukuzwa CCM, baadhi ya wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa nchini waliamini kuwa angemfuata Lowassa ambaye alikuwa akimuunga mkono walipokuwa CCM, hasa baada ya Lowassa kukaririwa katika waraka aliomtaka Simba na wengine waliotimuliwa CCM wahamie Chadema aliko yeye.
Hata hivyo, Simba hakumfuata Lowassa bali, alianza kufanya jitihada kadhaa za kuomba msamaha CCM na mwishowe dhamira yake hiyo kufanikiwa baada ya kutangazwa rasmi Ikulu jijini Dar es Salaam jana, kuwa amesamehewa na kurudishiwa uanachama wake wa CCM.
ALIVYORUDISHWA CCM

Kurudishwa kwa Simba CCM kulitokana na uamuzi wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, uliofanyika jana Ikulu jijijni Dar es Salaam.
Mkutano huo ulikubali ombi aliloliwasilisha Simba kwa njia ya barua iliyosomwa na mwenyekiti wa chama hicho, Rais Magufuli, ambayo ilionyesha kuwa aliandika Machi 14, mwaka huu.
Akisoma barua ya Simba, Rais Magufuli alisema alishakiri kufanya kosa hilo na kujuta kufanya hivyo na kueleza kuwa adhabu aliyopewa ilikuwa kubwa kwake na hawezi kurudia tena.
Katika barua hiyo, Simba pia alieleza kuwa ameamua kuiandikia CCM barua ili kuomba msamaha kwa sababu anaamini katika kuendelea kuwapo CCM na kwamba mali zote alizo nazo alizipata akiwa ndani ya CCM.
“Nimekukosea Mwenyekiti wangu, wajumbe wa NEC, Kamati Kuu na wanachama kwa ujumla. Adhabu niliyopewa nimeipokea kwa mikono mikunjufu. Nimekukosea mwenyekiti wangu na chama kwa ujumla,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.
Aidha, Simba alieleza kuwa adhabu aliyopewa ni mzigo mzito kwake na hajui jinsi ya kuubeba na kwamba ni adhabu ya kwanza kupewa na anaamini kuwa ni ya mwisho kwa sababu hatarudia tena.
“Naomba radhi tena, nisamehe sana, naomba huruma yako mwenyekiti na huruma ya wanachama,” ilieleza zaidi barua hiyo.
Akielezea kuhusu ombi hilo, Rais Magufuli alisema hakujibu barua alizokuwa akiandikiwa na Simba kwa sababu awali alikuwa akiangalia mwenendo wake na chama kimeridhishwa nao kwamba mkutano uliomfukuza ndio wenye mamlaka ya kumrudisha.
Wajumbe hao waliamua kwa sauti na kauli moja kumsamehe Simba na Rais Magufuli aliijibu barua hiyo kwa kumwandikia kuwa chama kimemsamehe.
Magufuli alisema kati ya wanachama waliowavua uanachama, ni Simba pekee ndiye aliandika barua ya kuomba radhi na wengine wawili waliandika barua ya kukubaliana na adhabu waliyopewa huku wengine wakikaa kimya.
Aidha, mwenyekiti huyo (Magufuli), alimtaka Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kumfikishia Simba ujumbe wa kumsamehe.
WALIOTIMULIWA CCM

Wakati Simba akivuliwa uanachama Machi, Adam Kimbisa alisamehewa kosa lake huku Emmanuel Nchimbi akipewa onyo kali. Wajumbe hao watatu wa Kamati Kuu ndio waliopinga waziwazi kuenguliwa kwa jina la Lowassa.
Wengine waliovuliwa uwanachama siku Simba alipoadhibiwa ni pamoja na waliokuwa Mwenyekiti wa Wilaya ya Kinondoni, Salum Madenge; Mwenyekiti wa Wilaya ya Ilala, Assa Simba; Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Christopher Sanya na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Ernest Kwilasa.
Wengine ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida; Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Jesca Msabatavangu; Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, Ali Sumaye na Mjumbe wa NEC Arumeru, Mathias Manga.

Advertisements
%d bloggers like this: