Skip to content
Advertisements

MATATIZO YANAYOMFANYA MWANAMKE ASIPATE UJAUZITO HARAKA

KWA kawaida mwanamke anatakiwa apate ujauzito ndani ya mwaka mmoja baada tu ya kuolewa au kuanza uhusiano. Tunategemea baada ya miaka miwili hadi mitatu baada ya kupata mtoto apate mwingine labda kama hajaamua yeye pamoja na mumewe. Ujauzito unapatikana baada ya kufanya tendo la ndoa kwa ukamilifu, yaani katika kipindi ambacho mwanamke anaweza kupata ujauzito wengine wanaita siku za hatari.

Suala hili pia linaangalia kwa upande wa pili wa mwanaume ambaye pia tunategemea ana uwezo huo wa kumpa mwanamke mimba kwa kuwa na mbegu zenye ubora na nyingi pia awe na nguvu za kutosha za kufanya tendo ili mwenzi wake apate ujauzito.
Kitendo cha kukaa muda mrefu bila ya kupata mtoto huku mkiwa mnamtafuta hitwa ugumba, kwa hiyo unahitaji uchunguzi na tiba.

CHANZO CHA MATATIZO
Mwanamke kutopata ujauzito husababishwa na matatizo mengi kwa upande wake au mumewe.
Kwa upande wa mwanaume vyanzo vinaweza kuwa kukosa nguvu kabisa au kupungukiwa nguvu za kiume, tatizo ambalo tayari tumelizungumzia katika makala zilizopita.
Mwanaume anaweza kutoa manii nyepesi sana kiasi kwamba baada tu ya kumaliza tendo mwanamke akisimama zinamwagika au zinatoka, dalili nyingine ni pale manii zinapopimwa hospitali na kuonekana zipo chache sana au hazina nguvu. Matatizo haya pia tayari tumeshayaeleza hapo nyuma.

Kwa upande wa mwanamke vyanzo vinaweza kuwa matatizo katika mfumo wa homoni au vichocheo mbalimbali vya uzalishaji mayai, upevushaji mayai, mzunguko. Mwanamke mwenye tatizo hili hupoteza siku zake za hedhi, mzunguko wa hedhi huvurugika na asijue ratiba yake ya mzunguko, hupoteza hamu na raha ya tendo, maumivu wakati wa tendo, hapati ute wa uzazi. Matatizo mengine ni kuziba kwa mirija ya uzazi, uwepo wa uvimbe katika mfuko wa uzazi, kupata damu ya hedhi kwa muda mfupi sana yaani moja au mbili au zaidi ya siku saba. Kuumwa tumbo chini ya kitovu mara kwa mara, kutokwa sana na uchafu ukeni ambao wakati mwingine huambatana na harufu mbaya na muwasho, maumivu wakati wa haja ndogo.

Matatizo ya kutokwa na uchafu ukeni na muwasho havihusiani na ugonjwa wa yutiai.
Matatizo mengine yanayomfanya mwanamke asipate ujauzito anapohitaji ni kutokufahamu siku za kupata mimba. Ili kufahamu siku za kupata mimba lazima ufahamu kwanza mzunguko wako uko vipi, mada hii tutakuja kuiongelea katika makala zijazo. Vilevile mwanamke ajue siku zake za “Ovulation” au siku za ute wa uzazi.

Ute wa uzazi upo wa aina tatu, kuna mwepesi, mwepesi na kuvutika na mzito. Ute wa uzazi ndiyo unaokuwezesha upate ujauzito. Suala la kufahamu mzunguko wa hedhi, siku za kupata mimba ni suala linalowahusu wote wawili, mume na mke.
Matatizo ya kisaikolojia kwa mwanaume na mwanamke pia huchangia tatizo hili, unene kupita kiasi kwa wote pia husumbua tatizo hili.

DALILI ZA TATIZO
Kama tulivyoona, kitendo cha mwanamke na mumewe kukaa zaidi ya mwaka wanatafuta mtoto ni tatizo kwa hiyo linahitaji uchunguzi na uchunguzi unafanyika pande zote mbili.

Mwanamke anayesumbuliwa na maumivu chini ya tumbo mara kwa mara naye yupo katika hatari hii kwani upo uwezekano wa kuathiri mirija yake ya uzazi na ikaziba kabisa, mzunguko wa hedhi unavurugika na kupoteza hamu ya tendo la ndoa.
Wanawake wengine hupata maumivu ya kiuno na tumbo kwa muda mrefu, siyo dalili nzuri. Matiti au chuchu kutoa maziwa pia huathiri kwa kiasi kikubwa uzazi kwani ni dalili kwamba homoni na inakuwa vigumu kupata ujauzito hasa kwa wasichana.

Maumivu wakati wa hedhi pia si dalili njema katika mfumo wa uzazi kwani inaweza kuwa una maambukizi sugu ya kizazi au “Chronic PID”, uvimbe katika kizazi au “uterine fibroid” au tabaka la ndani la kizazi kuwa nje. Hizi ni dalili chache kwa mwanamke.
Kwa upande wa mwanaume dalili pia zipo nyingi lakini kama nilivyoelezea hapo awali, ila kama mwanaume anashindwa kufanya tendo la ndoa hilo ni tatizo kubwa, maumivu ya njia ya mkojo, maumivu ya korodani, kutotoa kabisa manii pia ni mojawapo ya tatizo.

Mwanaume anaweza kupata matatizo ya uzazi endapo atavuta sana sigara na matumizi ya vilevi kwa muda mrefu hasa pombe kali na madawa ya kulevya.
Zipo dalili nyingine ambazo hazionekani wazi kwa mwanamke, mfano uwepo wa uvimbe kwenye vifuko vya mayai hali iitwayo kitaalamu “Polycystic Ovurian disease” huambatana na kufunga hedhi kwa muda mrefu hata mwaka, mwanamke huota vinyweleo vingi mwilini hasa miguuni, mapajani, mikononi, ndevu, hali iitwayo kitaalamu “Hirtuism”.

UCHUNGUZI
Hufanyika katika kliniki za magonjwa ya kinamama kwenye Hospitali za mikoa na rufaa. Muone daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi katika hospitali hizo akuchunguze. Epuka matumizi ya dawa bila ya kufanyiwa uchunguzi hospitali. Vipimo mbalimbali hufanyika kama vipimo vya damu kuangalia homoni na maambukizi mengine yanayokwamisha vipimo vya “Ultrasound”, mirija kiitwacho HSG na vingine ambavyo daktari ataona vinafaa.

Advertisements
%d bloggers like this: